DOGO AKIMSIKILIZA SILAA
MEYA wa Ilala , Jerry Slaa, amesema kuwa licha ya umoja wa
vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) kuonekana kuwa nguzo ndani ya chama
hicho, lakini ndiyo jumuiya inayongoza kwa migawanyiko na makundi ndani ya
chama hicho, inayochochewa na watu toka nje.
Slaa ambaye pia, ni mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC), kutoka
wilaya ya Ilala, amesema kuwa hali hiyo inakiweka rehani chama hicho, hivyo
kuwataka vijana hao wabadilike na kuacha kufanya siasa za mtu, bali wafanye
siasa za chama, kwani hiyo ndio suluhu itakayoiwezesha chama hicho kurudisha
imani kwa jamii.
Alitoa kauli hiyo jana, Jijini hapa, wakati akifungua semina ya
siku mbili ya viongozi 60 wa jumuiya hiyo, kutoka wilaya zote za mkoa wa Mbeya,
iliyoandaliwa mahususi kwa ajili ya kuwajengea uwezo viongozi kwa lengo la
kwenda kukijenga chama baada ya kumalizika uchaguzi wa ndani.
Alisema licha ya kwamba CCM bado inaaminiwa kwa kiasi kikubwa na
jamii, lakini bado kuna mambo muhimu ambayo chama hicho na jumuiya zake,
kinapaswa kuendelea kuyafanya ili kuendelea kukiimarishaya na kujenga imani
zaidi ndani ya jamii.
Hata hivyo , alisema wakati vijana hao wakifurahia kupata nafasi
za kushika madaraka mbalimbali, lakini pia wanapaswa kufikiria zaidi wajibu wao
kuanzia katuika sehemu wanazotoka hadi kwenye nyadhifa walizoshika, ikiwemo
kusimamia ipasavyo utekelezaji wa ilani ya chama hicho.
“Wewe kama kiongozi unapaswa kujiuliza ni kwa kiwango gani
umetimiza wajibu wako huko uliko (sehemu wakaoishi), lakini pia ni kiwango gani
umezisimamia halmashauri katika kutekeleza ilani ya chama” alisema Slaa.
Alisema kazi kubwa ya jumuiya hiyo na wana CCM kwa ujumula ni
kuunganisha nguvu zao kwa pamoja ili kuendelea kukijenga chama ili kiaminiwe na
wananchi na hatimaye kuendelea kupewa dhamana ya kuongoza dola.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi katika ufunguzi huo wa semina
elekezi kwa viongozi wa jumuiya hiyo, Mwenyekitti wa jumuiya hiyo Mkoa wa
Mbeya, Aman Kajuna, alisema vijana nchini wakiwemo wa CCM wanapaswa kuwa jicho
la mabadiliko hapa nchini.
Aliongeza kuwa vijana nchini wanatakiwa kuacha kuendesha mambo
na mipango yao kwa mazoea badala yake watekeleze hayo kulingana na mabadiliko
ya ulimwengu wa sasa na mahitaji ya jamii.
Baada ya kufungua semina hiyo ya siku mbili, MNEC huyo,
alifanikiwa pia kukutana na viongozi mbalimbali wa chama hicho na alitarajiwa
kufanya mkutano wa hadhara katika eneo la Nzovwe Jijini hapa.
Na Moses Ng’wat, picha na Mbeya yetu
|
0 comments:
Post a Comment